Askofu wa Kanisa la Good News For All Ministry, Dkt. Charles Gadi
ameipongeza Serikali kwa kushirikiana bega kwa bega na familia za wafiwa
na wananchi wa mkoa wa Arusha katika kuomboleza msiba uliotokana na
ajali iliyosababisha vifo vya wanafunzi 32, waalimu wawili na dereva wa
shule ya Lucky Vicent.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema hii
leo jijini Dar es salaam, amesema kuwa Kanisa lake linaungana na famili
za marehemu hao kuomboleza msiba huo mkubwa ulioacha simanzi kwa familia
na taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli imefanya kazi kubwa
kuwaunganisha wananchi wa mkoa wa Arusha na kuleta faraja kwa Watanzania
na familia zilizopoteza watoto wao.
“Tunaipongeza Serikali yetu ya Rais Dkt. John Magufuli kwa jinsi
ilivyouchukulia msiba huu kwa uzito mkubwa. Tumeguswa sana jinsi Makamu
wa Rais Samia Suluhu alivyoshiriki kwenye kuaga miili ya watoto hao.”
Amesema Askofu Gadi.
Hata hivyo, Katika hatua nyingine Askofu Gadi aliongoza maombi ya
kumuomba Mungu mvua iache kunyesha mkoani Dar es Salaam na ukanda wa
pwani badala yake Mungu aielekeze kwenye mikoa mingine ambako
inahitajika kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine.
Post A Comment: