Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’
imewashangaza vijana wa timu ya Taifa ya Ghana (U17) baada ya kuchomoa
mabao mawili katika dakika za nyongeza na kupata sare ya mabao 2-2
katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa
Taifa Dar es Salaam.
Mchezo huo ni wa mwisho kwa Serengeti hapa nchini kwani Aprili 5 timu
hiyo itaondoka kuelekea Morocco kwa ajili ya kambi ya mwezi mmoja kabla
ya kwenda Gabon kwenye michuano ya Afrika kwa vijana itakayoanza mwezi
ujao.
Sulley Ibrahim aliipatia Ghana bao la kuongoza dakika ya 21 kwa shuti
kali ndani ya 18 lililomshinda mlinda mlango wa Serengeti Ramadhan
Kabwili na kutinga wavuni.
Arko Mensah aliipatia bao la pili Ghana kwa mpira wa adhabu ndogo nje
kidogo ya 18 alioupiga kiufundi na kutinga moja kwa moja wavuni.
Serengeti walisawazisha mabao hayo katika dakika za nyongeza kupitia
kwa Assad Juma kwa mkwaju wa penalti kabla Muhsin Malima hajafunga bao
la pili mwishoni kabisa mwa mchezo.
Post A Comment: