Dj wa Clouds Fm, DJ D Ommy ambaye hivi karibuni alizindua kwa vitendo
mradi wake wa kuwakutanisha kwenye ngoma moja wasanii kadhaa,
amefunguka jinsi alivyounganisha wakali wa RnB halisi (Jux na Ben Pol)
na mkali wa ‘melodi’ za Bongo Fleva, Baraka Da Prince kwenye ngoma yake
‘DJ’.
Akizungumza na Dar24, DJ D Ommy amesema kuwa aliamua kuwakutanisha
wakali hao kwenye ‘DJ’ na kuwapa wazo la kufanya wimbo huo, kutokana na
hisia za muziki fulani uliokuwa unakuja kichwani kwake lakini bado
haujafanyika.
Alisema kuwa baada ya kuwakutanisha wakali hao aliwapa wazo na mdundo
ambao waliufanyia kazi usiku mmoja huku akisimamia hatua zote ili
kupata ile ladha ambayo alikuwa anahisi itawafaa mashabiki wake.
“Unajua lengo la projects zangu ni kuwafanya mashabiki wangu wapate
ladha ya muziki ninayohisi inatakiwa kuwepo lakini haipo kutokana na
sababu mbalimbali. Kwahiyo ‘DJ’ ni moja kati ya miziki itakayotokana na
hisia zangu za muziki na husimamia utayarishaji wake,” DJ D Ommy
aliiambia Dar24.
Katika hatua nyingine, DJ huyo ambaye ni mshindi wa tuzo ya DJ Bora
wa Afrika alisema kuwa tayari ameshakamilisha nyimbo zaidi ya 12 na kati
ya hizo ni pamoja na Bongo-Marekani kolabo.
“Kuna ngoma nimefanikisha kolabo kati na wasanii wa Marekani na
wasanii wetu wa Bongo. Itakuwa project kali sana na ya aina yake. Sitaki
kuweka kila kitu wazi sasa, lakini tusubiri muda utafika,” DJ D Ommy
aliiambia Dar24.
DJ huyo amepata mapokezi makubwa nchini Marekani ambapo mixing zake
zinasikika kwenye moja kati ya radio zinazorusha matangazo yake kwa
lugha ya Kiswahili, huku akipewa nafasi kwenye baadhi ya club za usiku
kwenye majiji makubwa nchini humo.
Post A Comment: