WAZIRI NAPE AWATAKA MAAFISA MAWASILIANO SERIKALINI KUTENDEA HAKI SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI

Share it:



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amewataka Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kuzisoma, kuzielewa na kuzifanyia kazi sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na ile ya Haki ya kupata Taarifa ya mwaka 2016 ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuuhabarisha umma.

Waziri Nape ameyasema hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa akifungua mkutano wa Maafisa Mawasiliano Serikalini ambapo licha ya kuwataka kuzijua sheria hizo pia amewataka kuwa wabunifu kuendana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika utendaji kazi wa kila siku.
Aidha aliongeza kuwa kuwepo kwa sheria hizo mbili kutatengeneza daraja litakalounganisha na kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa wananchi.

“Ni wajibu wa Maafisa Mawasiliano kuzijua na kuzitendea kazi sheria hizi ili kurahisisha upatikanaji wa mawasiliano baina ya serikalini na umma hivyo kuondoa ugumu uliokuwepo hususani katika kupatikana kwa taarifa muhimu kwa wananchi,” alisema Waziri Nape.

Aliongeza kwa kufafanua kuwa endapo utekelezaji wa sheria hizi mbili muhimu utasimamiwa na kuzingatiwa basi kutakuwepo na matokeo chanya ya kiutendaji na hivyo kuleta mafanikio makubwa yanayotarajiwa na umma.

Waziri Nape pia aliwataka Maafisa Mawasiliano hao kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuendana na maendeleo ya teknolojia ikiwemo matumizi ya mitandao ya kijamii katika kuhabarisha umma na kutoa taarifa kwa wakati.

“Zama hizi sio zile za maafisa mawasiliano kujisifia kwa kuwa na safari nyingi badala yake kuwa watekelezaji wa kazi zao kwa wakati na matokeo yanayoonekana kwa umma ila kwa atakayeshindwa kutekeleza hayo basi tutaomba atupishe,” alisema Waziri Nape.

Aidha alieleza kuwa anafahamu kuwa kuna changamoto nyingi ambazo maafisa mawasiliano wanakumbana nazo katika utendaji wao wa kazi ikiwemo ukosefu wa vifaa ingawa si kigezo cha wao kutokutekeleza wajibu wao.

Katika kuhakikisha kuwa changamoto ya ukosefu wa vifaa inatatuliwa Waziri Nape alitoa Wito kwa Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuweka kipaumbele katika bajeti hii mpya kwa kutenga kiasi cha fedha ambacho kitasaidia kununua vifaa kwa ajili ya Maafisa Mawasiliano wa Wizara, Taasisi, Mikoa, Wilaya na Halmashauri .

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao alisema kuwa umuhimu wa mkutano wa Maafisa Mawasiliano Serikalini ni katika kuwajengea uwezo wa kiutendaji pamoja na kutathmini utendaji kazi wao.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Elizabeth Simon Kitundu ameishukuru Wizara kuandaa mafunzo kwa Maafisa Mawasiliano Serikalini na kuyafanyia Dodoma kwani kwa kufanya hivyo itarahishisha mfumo wa kimawasiliano na kutangaza fursa zilizopo Dodoma hivyo kuwafanya watumishi wa umma kuwa na amani katika kutekeleza agizo la kuhamia Dodoma.

Mkutano wa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini umefanyika kwa mara ya 12 huku lengo ikiwa ni kuwakutanisha kwa pamoja maafisa hao kutoka katika ngazi mbalimbali za kiutendaji serikalini ikiwemo Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa, Wilaya na Halmashauri ili kuweza kubadilishana uzoefu wa kiutendaji pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Share it:

EAST AFRICA NEWS

Post A Comment: