MAKALA: WALIOTIMULIWA CCM KWA ‘USALITI’ NI MZIGO AU SILAHA WAKIHAMIA UKAWA?

Share it:
Ingawa maji ni ‘dhahabu’ jangwani, kuna wakati hata aliyebeba maji mengi jangwani hulazimika kuyapunguza ili mzigo wake ubebeke. Tendo hilo linaweza kutafsiriwa vibaya na mtu mwenye kiu anayelishuhudia kwa macho tu akiwa mbali bila kujua kinachomsibu aliyeamua kuyamwaga.
Lakini uamuzi huu unaweza kuwa rahisi zaidi kama aliyebeba maji hayo anaona kazidiwa zaidi na kidumu anachoamini kina ‘maji machafu’, ni dhahiri atakitupilia mbali bila kujali yuko katika jangwa kavu kiasi gani.
Jana, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliweka historia ya aina yake baada yakuwavua uanachama vigogo 12 wa chama hicho kwa tuhuma za usaliti, hali ambayo bila shaka imeacha nundu ya ubaridi wa hofu kwa baadhi ya wanachama na hewa nzuri ya matumaini ya chama safi zaidi kwa wengine.
Tunafahamu kuwa kati ya waliotupwa nje, yumo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho. Wengine ni wajumbe wawili wa NEC, Ally Sumaye na Erasto Manga. Fagio hilo la chuma pia liliwazoa wenyeviti wanne wa mikoa na watano wa wilaya, na wengine kupewa onyo. Sababu kubwa ikiwa kutiwa hatiani kwa USALITI.
Neno ‘usaliti’ lina maana kubwa ya harufu ya hatari nzito ya kuwauzia wapinzani au maadui siri za kambi kwa lengo la kuwapa ushindi. Kibaya zaidi, msaliti hujua siri nyingi za ndani na wakati mwingine zile ‘siri kubwa’ ambazo kwa lugha ya kigeni huitwa ‘top secrets’. Hivyo anapoamua kumpa adui ni kama anampa moyo wako aushughulikie.
Hakika msaliti ni zaidi ya sumu kali ndani ya mwili uliyoikoroga vizuri na kuinywa ukidhani ni supu nzuri ya kuongeza vitamini. Usipoiwahi itawahi kukuua!
Hata hivyo, ni dhahiri kuwa msaliti wako ni ‘malaika mpendwa’ wa adui yako. Ingawa wewe ulimchukulia kama mwanao, yeye ni zaidi ya mtoto mpendwa wa adui yako aliyejitolea maisha yake au kuweka rehani kazi yake kwa lengo la kumfaidisha huyo adui yako. Msaliti wako ni mtu ambaye ni rafiki yako lakini mtiifu zaidi kwa adui yako. Hivyo, kiuhalisia, hata kama unamlipa vizuri tambua ana maslahi zaidi kule kwa adui kuliko kwako.
Kwa ufafanuzi huo mfupi, naomba tuzame kidogo kwenye hili la wanachama waliobainika kuwa wasaliti ndani ya CCM, ambao ni dhahiri kuwa walibainika kufanya usaliti huo wakimuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyekihama chama hicho na kuelekea Chadema alikopewa nafasi ya kugombea urais akiungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa.
Kwa maana hiyo, watu hao walikisaliti chama hicho kwa lengo la kuifaidisha kambi ya Ukawa ambayo ni wapinzani wakubwa wa CCM na kwa mara ya kwanza walikipa chama hicho tawala wakati mgumu kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 kuliko wakati wowote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Baada ya kazi hiyo, wamebainika na kutimuliwa ndani ya CCM. Napata kiu ya kufahamu hatma yao nje ya chama hicho, wakiwa na picha ya usaliti.
Kwa wazo la harakaharaka, watu hawa kazi yao kuu na kipaji chao ni siasa. Hivyo, baada ya kuvuliwa uanachama wa CCM watakuwa na machaguo mawili tu, la kwanza ni kuhamia kule walikodaiwa kusaidia, yaani vyama vinavyounda Ukawa. Chaguo la pili ni kuacha siasa na kufanya mambo mengine. Nadhani chaguo la kwanza lina nafasi zaidi kwa watu hawa kwani maisha yao ni siasa. Wanaweza wasiamue leo lakini wakafanya baadae.
Je, endapo wataamua kujiunga na Chadema, CUF, NCCR Mageuzi au chama chochote cha upinzani, kupokelewa kwao kutakuwa na maana gani kwa vyama hivyo?
Kwanza, watu hawa watakuwa hazina kubwa kwa vyama hivyo kwani wamebeba siri, mbinu na uzoefu mkubwa kutoka CCM ambao utaweza kusaidia kuimarisha vyama hivyo.
Kwa mfano, ikitokea Sophia Simba akahamia Chadema, Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) litakuwa na nafasi ya kuchuma uzoefu na mbinu zitakazoujenga zaidi umoja huo, kwa kuzingatia kuwa UWT ni jumuiya kongwe zaidi ya wanawake nchini iliyopitia mengi na ina mafanikio makubwa. Kiongozi wake lazima awe mzinga wenye asali nzuri ya maarifa kwa BAWACHA.

Sophia Simba na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Dkt. Jakaya Kikwete (kutoka Maktaba)
Pia, Sophia Simba aliyewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM anaweza kuwa mzinga wa asali nzuri pia kwa upande wa pili kutokana na uzoefu wake na alichokibeba kuhusu CCM. Zaidi ya hapo, kama kiongozi wa jumuiya hiyo kubwa, lazima atakuwa na ‘connection’ yake pamoja na japo ka-kundi ka watu wanaomfuata na kumuamini. Hali kadhalika kwa wengine waliofukuzwa.
Kingine cha kufikiria kama sababu za kupokelewa kwao Ukawa, kama ni kweli walikuwa ‘wasaliti’, basi hawa walikuwa watoto wapendwa wa Ukawa waliokuwa wanalishwa na kunyweshwa na CCM. Hivyo, kuhamia Ukawa watakuwa sehemu nyingine sahihi kwao.
Sababu ya mwisho ya utetezi wa kubariki safari ya wasaliti wa CCM kwenda Ukawa, ni kwamba siasa ni mchezo wa namba kama alivyowahi kusema mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Idadi ya wanachama au watu ndio mtaji wa chama chochote cha siasa.
Hata hivyo, ili watu hao wawe hazina kweli, wanapaswa kufanyiwa uangalizi, kufunzwa miiko ya chama na kuwekwa kundini, lakini kuwa chini ya uangalizi maalum kwa kipindi fulani, kwani ingawa wanaweza kuwa na hasira dhidi ya CCM, inaweza kuwa vinginevyo.
Katika hatua nyingine, kuwapokea watu hawa ni kuongeza hatari ndani ya chama husika pia. Niliwahi kumsikia bibi yangu akisema kwa lugha ya nyumbani kuwa ‘Mlogi atakuta-agaye’. Kwa tafsiri ya maana ni kwamba ‘mchawi haachi asili yake… hata akienda ukweni ataruka tu!’. Wasaliti hawa, wanaweza kugeuka kuwa wasaliti wa Ukawa katika siku za baadae. Kwa wale waliosoma kuhusu mbinu ya kivita iliyowahi kutumiwa na falme moja kuangamiza falme nyingine iliyoitwa ‘Trojan Horse technique’ mtaelewa zaidi.
Sababu nyingine inayoweza kuunga mkono kutowapokea ni kujiridhisha kuwa sio tu kuongeza idadi ya watu, bali kuongeza idadi ya watu wasafi ndani ya chama ili kisichafuke bali kizidi kung’aa. Watu hawa wametajwa kukiuka kwa kiasi kikubwa maadili ya chama chao, sasa unapowapokea unaweza kuwa umewapa kichaka cha kuendelezea tabia yao badala ya kujirekebisha.
Lingine ambalo ni muhimu zaidi, ni taswira ya chama husika. Chama kitakachowapokea lazima kikutane na changamoto nzito dhidi ya taswira yake kuwa wamepokea makapi au kama CCM walivyosema wakati wa uchaguzi mkuu uliopita kuwa ‘reject’ ndio waliohamia Ukawa.
Mwisho, napenda Chadema na vyama vingine vya upinzani, kabla ya kuwapokea waliotimuliwa CCM kulikumbuka swali aliloliacha Dkt. Wilbroad Slaa (Aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema), “Mnawapokea kama ‘Asset au Liability’, kwa tafsiri isiyo rasmi ‘ni mali au mzigo’?
Share it:

EAST AFRICA NEWS

Post A Comment: