Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam jumanne ya Machi 13, 2017 katika eneo la Mongo la Ndege, limeokota mwili wa mtoto wa kike aliyefahamika kwa jina la Imelda Ngonyani (13) aliyekufa maji wakati akijaribu kuvuka mto Msimbazi.
Akiuzungumza na waandishi wa habari Machi 14, 2017, Kamishna wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro amesema marehemu huyo kabla ya kufa maji alikuwa pamoja na wenzake watano walionusurika kifo wakielekea shule ya Msingi ya Mongo la Ndege.
“Mwanafunzi huyo alikufa maji wakati akijaribu kuvuka mto Msimbazi akiwa na wenzake ambao walinusurika kifo wakiwa njiani kuelekea shule ya Mongo la Ndege,” amesema.
Sirro ametoa wito kwa wananchi kuwa makini katika kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea kunyesha, na kuwataka wananchi wanaoishi karibu na mto msimbazi kuondoka kwa hiari ili kujiepusha na athari za mafuriko.
Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro amesema Jeshi la Polisi mnamo Machi 12, 2017 maeneo ya Zimbwini kata ya Vijibweni Manispaa ya Kigamboni lilifanikiwa kukamata watuhumiwa wawili wenye umri kati ya 25 hadi 30 wakiwa na bastola moja aina ya Bereta yenye risasi sita ndani ya magazini.
“Majambazi hao walijeruhiwa vibaya ndipo wakakimbizwa hospitali ya vijibweni, walipofikishwa hospitalini hapo walibainika kuwa wamefariki dunia wakiwa njiani. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa silaha hiyo iliyokamatwa ni mali ya Pato Sixtus Nyagali mkazi wa Kijichi, upelelezi unaendelea kufanyika ili kumpata mmiliki huyo na kuhakikisha mtandao wote wa uhalifu unafikishwa katika mkono wa sheria,” amesema.
Sambamba na hilo, Sirro amesema Kikosi cha Polisi Usalama Barabarani cha kanda hiyo, kimekusanya 319,350,000 za faini kwa ajili ya makosa mbalimbali ya barabara kuanzia Machi 10 hadi 13, 2017.
Post A Comment: