Rais wa Tanzania John Magufuli amesema kuanzishwa kwa mfumo mpya wa serikali wa ukusanyaji kodi kwa njia ya Kielekroniki, (Data Center) itakuwa dawa kwa wale wote wanaokwepa kulipa kodi.
Akizindua uanzishwaji wa mfumo huo, jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema ili kuondoa malalamiko ya wale wanaodai kubambikiziwa kodi isiyo sawa na wale wanaokwepa kulipa kodi, ufumbuzi ni kuwepo kwa kituo hicho.
Amesisitiza kuwa ni lazima kila mmoja alipe kodi, ili kuweza kupata mapato yatakayoweza kutumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya nchi.
Aidha ameyataka makampuni mbalimbali yaliyoko nchini, yakiwemo ya simu, na Wizara zote kuingia katika mfumo huo mpya wa serikali wa ukusanyaji kodi kwa njia ya kielekroniki, ambao ni muhimu wa ustawi na maendeleo ya nchi.
Rais Magufuli pia amesema kuanzisha kwa mfumo huo ni ukombozi wa kupunguza kero za muungano.
''...Kwa sababu ukijaza vocha yako huko Zanzibar hiyo pesa itaenza Zanzibar, ukinunulia vocha yako Kigoma au Moshi hiyo pesa itakuja TRA Tanzania bara , hakuna mabishano, chombo hiki kinagawa chenyewe ndio faida yake...'' amesema Magufuli.
Serikali imesema imejenga kituo hicho kwa ajili ya kulinda usalama wa taifa na taasisi za zake pamoja na makampuni binafsi yanayoendesha shughuli zao nchini.
Lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ni dhamira ya serikali ya Tanzania katika kukuza na kuimarisha sekta ya Teknolojia na Habari na mawasiliano ambayo inakuwa kwa kasi ulimwenguni kote na ni kichocheo kikubwa cha uchumi.
Post A Comment: