BARCELONA, ALAVES KUFUNGA UWANJA WA VICENTE CALDERON
Shirikisho la soka nchini Hispania (RFEF), limeutangaza uwanja wa Vicente Calderon kuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali ya kombe la Mfalme ambao utazikutanisha FC Barcelona na Deportivo Alaves, Mei 27.
RFEF, wametangaza mchezo huo kufanyika uwanjani hapo, kwa kuamini unatosha kukidhi haja ya mashabiki 55,000 watakaopata nafasi ya kuushuhudia, huku wakiwa wameketi vitini.
Hata hivyo mchezo huo wa fainali ya kombe la Mfalme utatoa heshima za mwisho kwenye uwanja wa Vicente Calderon unaomilikiwa na klabu ya Atletico Madrid tangu mwaka 1966, kufuatia dhamira iliyowekwa na uongozi wa klabu hiyo.
Atletico Madrid wanautumia uwanja huo kwa mara ya mwisho msimu huu, kabla ya kuhamia kwenye uwanja wao mpya utakaoitwa Wanda Metropolitano.
Mchezo wa fainali ya kombe la Mfalme, utakua wa mwisho kuchezwa uwanjani hapo kabla ya mageti yake kufungwa rasmi.
Post A Comment: