Serikali imesema itatoa eneo linalomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Buhemba, Mkoani Mara kwa wachimbaji Wadogo wa Madini baada ya kufanyika kwa tathmini na taratibu za kumilikishwa eneo ili wachimbaji hao wafanye shughuli hizo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ikiwemo kulipa kodi.Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo leo tarehe 18 Februari,2017, wakati wa ziara yake katika mgodi huo ili kuangalia shughuli za uokoaji zinazoendelea katika mgodi huo, kufuatia ajali ya kufukiwa na kifusi kwa Wachimbaji 18 iliyotokea tarehe 13 Februari,2017, ambapo wachimbaji 13 waliokolewa siku hiyo hiyo
Prof. Muhongo amesema kuwa, wachimbaji hao hawakuwa na leseni wala vibali halali vilivyotolewa kwao kufanya shughuli za utafutaji dhahabu na kwamba eneo hilo linamilikiwa kisheria na STAMICO kwa leseni PL N0. 7132/2011, na kuongeza kuwa, wachimbaji hao walivamia eneo hilo ambapo ni kosa kisheria na wanatambulika kama wavamizi.
Ameongeza kuwa, shughuli za uchimbaji katika eneo hilo zilifungwa tangu mwaka 1971 ambapo awali eneo hilo lilikuwa chini ya wakoloni kabla ya kuwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kampuni ya Meremeta na baadaye kuwa chini ya umiliki wa STAMICO.
Aidha, amezuia shughuli zote za uchimbaji kufanyika katika eneo hilo na kusema kinachofanyika sasa ni kuutafuta mwili wa mchimbaji mmoja ambaye bado haujatolewa. ''Hadi sasa wachimbaji 15 wamekwisha okolewa, bahati mbaya wawili walitolewa wamefariki na sasa tuendelee na zoezi la kutafuta mwili uliobaki,"ameongeza Prof. Muhongo.
Post A Comment: